KUNI MBICHI!
Kuni
mbichi ni msaliti wa moto. Torati zake ni kuufilisisha moto halafu kumshawishi
chakula asihusiane na binadamu. Majipu yalikuwa yameshauteka mwili wangu nyara
pasi huruma yoyote. Japo nilijizatiti niyakwaruze kwa, maji nayo yalikuwa
yashamwagika na bila shaka kiu iliyonigubika ilizidi kuninyonga hata karibu
nigeuke mwehu. Maisha nayo yalikuwa yametukodolea macho utadhani ibilisi
alikuwa akiyaongoza. Chakula nacho kilikuwa nadra ja maji jangwani. Kuparara kwetu
nako kulikuwa jambo jingine la kuzungumzia kwani macho yatakulipuka kwa
mshangao ndugu. Miili yetu ilikuwa imebaki mifupa hata ladha ya kuwa binadamu
ikawa shubiri. Kweli dunia si gunia la kuchezea ndugu na asiye na mwana atazame
uhondo wa mchafuko wa kimazingira ya kibin-mateso dhidi ya sanamu wa
kibin-adamu. Maisha nayo ni mshikomshiko na ukishikwa nawe shikamana na hiyo ni
tahadhari kwako. Tumbo langu je? Lim’baki upara ambao umechuchumaa kwa undani
kana kwamba laomboleza kifo cha shibe.
Jamani
mbona mimi na wenzangu tuteteseke hivi ilhali wengine wasaza hadi vyakula
vyatupiliwa mbwa vile? Kumbuka tunaye rafiki aliyetuhutubia kwa wak’ti mmoja
akiomba msaada wetu. Kwani ni msaada gani bwana Micah we? Aah! Ulikuwa msaada
mdogo jamani wa kimakaratasi tu. Yaani KURA shoga! Kwa kweli hilo lilikuwa
jambo dogo sana lisilohitaji hata hotuba yoyote kuliomba. Baada ya kupewa mapeni
ambayo yaliisha kwa kitumbo usiku huo tuliweza kushawishika kiubongo na tukampa
zote bila ya huruma yoyote. Wanadamu wamekuwa hayawani hata kwa nduguzo kwani
wamewafanya limbukeni wa kuwalamba miguu yao iliyojaa funza. Twawalamba hao
watu hadi uparani na katu hawatupatii mkono wa buriani. Mema wanayowafanyia
wananchi wenye dhiki ni kuwalaani kwa yoyote wanayoyafanya pasi hofu yoyote. Tumekuwa
watumwa wao jambo ambalo limewapa kiburi cha jogoo la boma asiyekuwa na moyo wa
kifalme wa nipe nikupe.
Hadhira
yetu imekuwa milki yao ya kutusomba namna wanavyotaka huku pia shida zetu
wanazipigia hesabu za tano ondoa sita! Kwa kweli misumari tuliyosulubiwa nayo
ni wao wanasiasa walinunua kwa minajili ya kutugandamanisha katika dhiki zetu.
Ehee! Maisha kizungumkuti! Imekuwa ajabu ya punda kujiwekelea mzigo halafu tena
ahitaji abebwe kwa gari na huo huo mzigo wake. Tumekuwa viumbe wanaojitumbukiza
kwa shimo tulionalo halafu baaye twahitaji mkono wa ibilisi utuokoe.
Kwangu maisha
yamekuwa mazito hata kuyamiliki yamekuwa mzigo mwingine. Nimekuwa mpokezi wa
misaada hadi wanaoileta wamechoka nami kwani nimekuwa kama mzigo kwao pia.
Tangu utotoni nimekuwa nikiishi kambini kwa wakimbizi hata kwetu halisi sipajui
wala siwezi kupafikiria kamwe. Kila uchao, wanasiasa hutupa sampuli ya vyakula
kusomba akili zetu. Chakula hiki kama kawaida huwa hakina ladha wala shibe
yoyote bali huwa ni cha kunifanya nisisahau ya kwamba kuna NGELI YA CHAKULA. Maishetu
yamekuwa parakwanja ya matatizo yas’okuwa na kikomo.
Lililonibakia
ni sala pekee kwa Rabuka mwenye kuumba na kutuneemesha kwa yoyote yale. Kichapo
cha Mola ndicho kitakachotuokoa kwa hawa ndugu zetu wenye fitina na njaa ya
makuu bila jasho. Humu duniani hakuna fimbo inayoweza kuwachapa kwani hata hizo
fimbo ni wao ndio walizozipanda kwa mashamba yao ya miswada onevu. Kwa sasa
nimebaki mnyonge lakini matumaini yangu ya kufika ng’ambo ile nyingine bado
haijadidimia kamwe. Bado najipa moyo. Siasa ni unyevu ilhali wanasiasa ni mbao
kwa hivyo siasa za wanasiasa ni KUNI MBICHI! La kunitia moyo sana ni ile tanuri
nionayo ng’ambo ile! WAKENYA TUTAFIKA!
Comments
Post a Comment