SIASA CHAFU
Hizi ndizo
nyakati ambazo cheche za maneno zilizouchi na zisotimilifu zitamwagwa hapa na
pale kwa watu wenye kiu kama mimi na wewe. Humu nchini usishangae kuwaona
vigogo wa kisiasa wakijikusanya kwa misingi ya kikabila pasi kuzingatia misingi-endeleo
ya nchi. Wanasiasa ni watu ambao wanamaradhi ya sintofahamu bin sahau na hata
baada ya machafuko yal’oshuhudiwa miaka ya 2007/2008 hawakushtushwa hata ncha. Mwanasiasa
ni pandikizi la mtu ambaye huwa mwingi kwa wakati fulani ilhali baadaye
huadimika. Anapokuwa kwa ombaomba zake huonekana kama ambaye anashida nyingi
zinazomnyonga na kumsomba kiakili. Nyakati hizo huonekana mwehu kwani ahadi
wanazotupa huweza kumchanganya hata Mola mwenyewe. Wanaweza kukuahidi ahera
japo wao ni familia ya jahanamuni. Kawaida hawa ni viumbe wal’otumwa na shetani
kuutwaa ulimwengu kupitia porojo zao zilizojaa fitina na ufidhuli mwingi sana. Siasa
ni kama biashara au uzinifu kwani sheria zake ni za nipe nikupe yaani nipe
karatasi yako ya kura nami nikuhutubie ulaghai wangu.
Kimwili huwa ni watu wenye miraba minne. Vitambi
hivi huashiria ule unafiki wa hali ya juu kwani watu wa eneo bunge lao huwa
wamechotwa kwa mikiki ya njaa na maradhi tetemesha. Uchi wa mwanasiasa ni
hadhara kwa yeyote na licha ya hayo bado sisi hujipata tumewachagua tena. Hili
huashiria namna wao hutumia dumba kwa kutusomba kimawaza. Kwa wakati mmoja
mganga mmoja alikiri kuwa wateja wake wakuu ni wanasiasa haswaa wa hapa nchini
Kenya. Jambo hili laonyesha namna walivyowasherati hawa wadhalimu. Kwa kawaida
utawapata wakiokoka katika mikutano ya injili ovyo ovyo. Hata Mungu naye
amekuwa adinasi wa kuchezewa na hawa wahalifu. Mikutano au hata janga lolote
linapotokea huwa hawaachwi nyuma. Binadamu wengine sio watu. Ukiwa na kitu
watakuja na unapokosa watakukimbia. Unapokuwa na kura watakukujia na unapokosa
kura hiyo huku ukiwa unateseka watakukimbia hawa wanasiasa. Huu si uungwana
hata kidogo!
Huwa twawaona mashujaa hao wanasiasa ilhali
hatuelewi ulimwengu wao. Haya huwa ni mapenzi bandia ambayo baadaye hutuelekeza
futi sita udongoni. Ulimwengu wao ni majabali ya miamba ya vyuma ambao chini
umesitiriwa na vigae vya vioo ambao bilashaka waashiria pengo la kutokuwa
kamilifu. Jasho la riziki yetu limekuwa dimbwi lao la kujistarehesha. Matendo
yao huashiria ule ukungu wa hewa yao chafu ulivyotanda himaya ya nchi yetu. Hata
mimea wameikosea kwa namna wanavyopitisha miswada inayoathiri misitu yetu
iliyoshwari.
Kwa wale ambao wanania ya kujitosa katika ulingo wa
kisiasa humu chuoni nawaomba mjichunguze kimienendo halafu jifokee ukiwa waona
hujiwezi. Ukiwa umeoza jipeleke makavazi kwani huo ndio ulimwengu wako. Nanyi
wapiga kura wenzangu pia tuwachunguze hawa adinasi ambao hutaka utajiri kwa
uongo kwa kuangalia kwa umakini ukucha wao hadi unnywele ule wa mwisho. Hawa
watu ni tisho kwa maisha yetu na wasipochunguzwa kwa umakini nasi tutaoza kama
wao kwani samaki mmoja akioza………..! wataja tuambukiza ngoma yao kwani hata
huruma hawana. Wamekuwa kama panya wanaokuuma kasha wanakupuliza. MAJINAMIZI!
Comments
Post a Comment